HALMASHAURI ZAFUNDWA MBINU ZA UJUMUISHI WA MASUALA YA UHIMILIVU NA MABADILIKO YA TABIANCHI KWENYE MIPANGO NA BAJETI
Na Andrew Mallya, Morogoro
Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI kinatekeleza Mradi wa Mabadiliko ya Tabianchi unaofadhiliwa na Mfuko wa Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF - LoCAL). Katika kutekeleza mradi huu, Chuo cha Mipango kinaendesha mafunzo kwa wataalamu wa serikali za Mitaa kutoka Halmashauri nane zinazonufaika na mradi huu.
Akiongea siku ya kwanza ya mafunzo haya yanayofanyika Ukumbi wa EDEMA , Manispaa ya Morogoro mratibu wa mafunzo haya Profesa Omari Mzirai amezitaja halmashauri hizo kuwa ni pamoja na Mpwapwa, Kondoa, Chamwino, Mkinga, Mafia, Mtwara, Mtama na Kigamboni.
Kwa mujibu wa Profesa Mzirai lengo la mafunzo haya ya siku nne ni kuwajengea uwezo wataalamu wa Serikali za Mitaa katika kujumuisha masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na uhimilivu katika Mipango na bajeti za Halmshauri zao.
Washiriki wa mafunzo haya ni wataalamu kutoka idara mbalimbali za Halmashauri ikiwemo Mipango, Fedha, Kilimo, Uvuvi, Mifugo na waratibu wa Mradi wa LoCAL kutoka katika Halmashauri shiriki.
Wawezeshaji wa mafunzo haya ni Profesa Omari Mzirai, Profesa Innocent Zilihona, Dkt. Christina Geofrey pamoja na Dkt. Aron Bakari. Wengine ni Bwana James Maghori, Bwana Sostenes Nakamo, Bi Fausta Senga na Bi Neema Nnko