Na Mariam Mayunga
Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini wametoa msaada wa vifaa vya ujenzi kwa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Kibaigwa kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa choo cha sokoni.
Alikabidhi msaada huo Mkurugenzi wa Taaluma Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Dkt. Maseke R. Mgabo amesema msaada huo ni kurudisha shukrani kwa jamii ya Kibaigwa kwa kuwaruhusu wanafunzi wa Chuo hicho kufanya mafunzo kwa vitendo katika mji huo. Vifaa vya ujenzi vilivyotolewa ni mifuko 40 ya saruji, bati 12, misumali ya nchi 4 kilo 5, mbao 10, white cement, na ndoo mbili za rangi.
''Tunaomba mpokee msaada huu japo ni mdogo ikiwa ni ishara ya kurudisha katika jamii sehemu ya mapato yetu na tumechagua kutoa vifaa vya ujenzi ilikuunga mkono jitihada za mamlaka ya mji mdogo wa Kibaigwa wa kuwa na choo cha kisasa sokoni ambapo kitahudumia watu wengi" alisema na kuongeza " tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kuchangia katika maeneo tofauti tofauti kadri uwezo wa kifedha utakavyoruhusu kwa minajiri ya kutoa mchango wetu katika kutatua changamoto za kimaendeleo zinazoikabili jamii yetu ya watanzania " alisema Dkt. Mgabo.
Akipokea msaada huo Afisa Mtendaji wa Kata ya Kibaigwa katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kibaigwa Bi. Foska Ernest Mgovano anaushukuru Uongozi wa Chuo cha Mipango kwa msaada walioutoa kwani kwa kiasi kikubwa utasaidia kupunguza changamoto waliyokuwa wakikabiliana nayo ya ujenzi wa Choo cha Gulio Kata ya Kibaigwa. Msaada huu umekuja kwa wakati mwafaka ambapo tulikuwa tunahangaika namna ya kupata vifaa vya ujenzi kukamilisha ujenzi wa choo kwenye gulio letu. Tunawashukuru sana".
Wanafunzi wa Chuo cha Mipango katika kutekeleza matakwa ya mitaala yao inayowataka wanafunzi kuwa mahiri kimeweka utaratibu wa wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo kwa muda usiopungua siku nane ambapo mwisho wa mafunzo hutakiwa kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Kijiji au Kata kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada mtawalia. Kwa upande wa wanafunzi wa shahada za kwanza hutakiwa kuandaa Hali ya Kiuchumi na Kijamii ya Wilaya na wale wa Shahada za Umahiri huandaa Mpango Mkakati wa Kisekta.
#Kupanga ni kuchagua!