TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA VYAMA VYA USHIRIKA NCHINI; Prof. Nkonoki
Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa - Mwanza, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof. Juvenal Nkonoki amesisitiza kuwa Chuo kitaendeleza ushirikiano na vyama vya ushirika vya SACCOS vilivyopo nchini katika kutatua changamoto za usimamizi wa vyama hivyo.
Amebainisha hayo Jumatatu Mei 19, 2025 katika hafla ya kufunga mafunzo ya Uongozi na Usimamizi Endelevu wa SACCOS yaliyofanyika kwa viongozi wa vyama vya ushirika SACCOS wa Wilaya ya Bunda yaliyofanyika kwa siku tano kuanzia Mei 15, 2025 hadi Mei 19, 2025 ambayo yameratibiwa na Chuo cha Mipango kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
“Chuo cha Mipango kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mtaifa (UNDP) tutaendelea kushirikiana na vyama vya ushirika nchini katika maeneo mbalimbali ya kiufanisi katika kuhakikisha vyama vya ushirika vinasongambele kwa weledi mkubwa hususani katika usimamizi wa vyama”. Alisema Prof. Nkonoki na kuongeza “tutajitahidi kadri tunapo pata nafasi kuyafikisha mafuzo haya kwa viongozi wote wa vyama hapa nchini katika mafunzo ya uongozi na usimamizi endelevu wa vyama vyetu”.
Aidha,Prof. Nkonoki amewataka viongozi hao kufikisha mrejesho wa mafunzo hayo kwa wanachama kwa wakati ili kuweza kutatua changamoto zilizopo katika vyama vya kuweka na Kukopa maarufu SACCOS.
Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo Bw. Charles Malunde amesema baada ya mafunzo hayo kwa viogozi hao anaamini kutatokea mabadiliko chanya ya kiutendaji kwa vyama hivyo vilivyopo wilayani Bunda kwani kwa mafunzo aliyo yatoa yanaenda kuleta msingi wa kiutendaji kwa ngazi zote katika vyama kuanzia kwenye mabaraza ya vyama hadi watendaji wa vyama.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Kibara Biashara SACCOS Bw. Hamadi Hamis Nyamanda kwa niaba ya wanachama wa Wilaya ya Bunda amekishukuru Chuo cha Mipango kwa uratibu na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ufadhili wa mafunzo hayo kwa vyama vya ushirika .
“kwa namna ya kipekee kabisa kwa niaba ya vyama vya ushirika Wilayani Bunda tunawashukuru mmno wawezeshaji pamoja na wafadhili wa mafunzo haya. Ninaomba kuendelea huahidi kuwa kuna mengi tunakwenda kuyafanyia mabadiliko katika vyama vyetu na vingi vinaenda kubadilisha vyama vyetu kiutendaji na kiutawala na hivyo ninapenda kutumia fursa hii kuahidi kuwa maazimio haya ya leo tunaenda kuyafanyia kazi kwa vitendo tukitumia weledi mkubwa” Alisema Bw. Nyamanda.