Mradi wa Bahari Maisha unaotekelezwa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) unatarajiwa kuongeza ushindani katika soko la mazao bahari kimataifa.
Hayo yamebainishwa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa Tanzania (UNDP) Bw. Shigeki Komatsubara katika hafla ya kukabidhi makaushio na mashine za kusaga zao la mwani, pamoja na vifaa vya kuwawezesha wakulima wa mwani, na wafugaji wa jongoo bahari na kaa iliyofanyika Ijumaa Oktoba 25, 2024 katika viwanja vya Jengo la Umoja wa Mataifa (UN House) Jijini Dar es salam.
Bw. Komatsubara amesema kupitia Mradi wa Bahari Maisha changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakabili wakulima wa mazao bahari kupitia mradi huu Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limechukua hatua kwa kufadhili mafunzo ya uendeshaji wa kilimo; usimamizi wa vikundi; usimamizi wa fedha; kuongeza thamani ya mazao pamoja na masoko kwa vikundi vya Wanawake na Vijana.
“Leo tunatoa mashine nne zenye uwezo wa kusaga zao la mwani tani moja kwa saa na makaushio manne yenye uwezo wa kukausha mwani tani moja kwa mara moja pamoja na bando elfu mbili za kamba na bando elfu tatu za taitai ili kuwawezesha wakulima wa mwani na wafugaji wa kaa na jongoo bahari katika maeneo ya Tanga, Bagamoyo, Unguja na Pemba kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao haya kimataifa". Alisema Bw. Komatsubara.
Vilevile, Bw. Komatsubara amebainisha kuwa Shirika linaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wadau mbali mbali wa maendeleo kuinua Uchumi wa Bluu hususani kwa makundi ya wanawake na vijana.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuweka mkazo wa Uchumi wa Bluu, ambapo amebainisha kuwa Mkoa wa Tanga unaendelea kuimalisha uvuvu salama na kuhamasisha kilimo cha mwani pamoja na ufugaji wa jongoo bahari na unenepeshaji wa kaa. Vile vile amehimiza matumizi ya teknolojia ya kisasa katika zao la mwani ili kupata bidhaa mbali mbali zenye ubora.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kepteni Hamad Hamad amelishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamojana Chuo cha Mipango kwa mradi huo kwani unawagusa moja kwa moja kiuchumi Wananchi wa Zanzibari.
Pia Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Edwin Mhede amebainisha kuwa uzalishaji wa zao la mwani unaendele kukua kutoka tani elfu tatu mwaka 2021 hadi kufikia tani elfu tisa kwa mwaka huu 2024 ikiwa ni ongeezeko la asilimia 166.67, hivyo kwa niaba ya Serikali ameahidi ushirikiano madhubuti kwa wadau wa maendeleo.
Awali akitoa taarifa ya utakelezaji wa Mradi huo wa Bahari Maisha Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Juvenal Nkonoki amesema mradi huo unaotekelezwa na Chuo ni matokeo ya tafiti iliyofanywa kwa wakulima wa mazao bahari na kubaini changamoto kadhaa zinazowakabili wakulima hao. Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na mbinu duni na ukosefu wa vifaa vya kisasa. Hivyo, Chuo kwa kushirikiana na UNDP waliandaa programu maalumu ya mafunzo elekezi ya uendeshaji wa kilimo kisasa; usimamizi wa vikundi; usimamizi wa fedha; kuongeza thamani ya mazao pamoja na masoko ambapo zaidi ya wakulima na wafugaji 350 wa mazao bahari katika maeneo ya Unguja, Pemba, Tanga, na Bagamoyo wamenufaika na mafunzo hayo.