Na Mariam Mayunga - Mwanza
Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Hozen Mayaya amewaasa Watumishi wa Chuo Cha Mipango Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa - Mwanza kujiunga na vikundi mbalimbali vya kijamii vilivyopo chuoni, kwani kupitia vikundi hivyo wanachama hupata manufaa mengi ikiwemo kusaidiana wakati wa raha na shida na kuimarisha mahusiano miongoni mwao.
Rai hiyo ameitoa Juni 21, 2024 katika kikao cha ndani cha Watumishi wa Chuo cha Mipango, Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa - Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
"Mpaka sasa tuna jumla ya Watumishi 438 lakini wengi hatujajiunga na vikundi mbalimbali vya kijamii vilivyopo hapa chuoni. Nawaomba viongozi wa Vikundi kutoa gharama za viingilio ili kupata wanachama wengi" alisema na kuongeza " tunavyama vingi: Chama cha Wanataaluma Chuo cha Mipango (MIASA); Chama cha Wafanyakazi Mipango (CHAWAMI) Umoja wa Wanawake Mipango (UWAMI), MIPANGO SACCOS, na Vyama huru vya wafanyakazi THTU na RAAWU" alisema Profesa Mayaya.
#Kupanga ni Kuchagua