Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kimetoa misaada mbalimbali kwa shule za Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Tukio hilo limetokea Alhamisi Juni, 6 wakati Mkuu wa Idara ya Fedha za Maendeleo na mafunzo ya uongozi Dkt. Judith Namabira alipofanya ziara kukagua maendeleo ya wanafunzi wa Chuo hicho waliokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo katika kata za Kidoka, Chemba, Paranga na Gwandi.
Shule zilizonufaika ni pamoja na Shule ya Msingi Kidoka na Shule ya Msingi Kelema Balai zilizopata mifuko 20 ya saruji kila moja. Shule ya Msingi Chemba imepata viti 13 vya walimu na meza moja ya mwalimu mkuu wakati Shule ya Msingi Gwandi imepata vifaa vya umeme vya thamani ya laki tano.
Chuo cha Mipango kimetoa Misaada hiyo ikiwa ni kurudisha fadhira kwa maeneo hayo ambayo wanafunzi wa Chuo hicho walikuwa kwenye mafunzo kwa vitendo .
"Katika ziara yake hiyo iliyoambatana na utoaji wa misaada Dkt. Namabira amewaasa wanafunzi wa Chuo cha Mipango kudumisha maadili mema kwa kipindi chote wakiwa kwenye mafunzo kwa vitendo wilayani Chemba. " Endeleeni kufanya kazi kwa bidii na kutanguliza huku mkionesha kwa vitendo nidhamu ya hali ya juu kwa jamii mnayofanya nayo kazi kwani jamii hii ni sehemu ya jamii kubwa ya watanzania ambayo mnategemewa kwenda kuitumikia" Alisema Dkt. Namabira
Naye Diwani wa kata ya Paranga Mhe. Ngwandi Kimolo Chobu ameushukuru uongozi wa Chuo cha Mipango kwa misaada mbalimbali ambayo imekidhi mahitaji ya shule zao. " Ninauombea heri uongozi wa Chuo kwa hisani waliyotufanyia" alisema Mheshimiwa Chobu.
Akielezea juu ya mafunzo hayo mmoja wa wanafunzi wa Chuo cha Mipango Bi. Mwajuma Zawadi Samwel alisema "Mafunzo haya yametupa mbinu za medani za utendaji wa kazi zetu. Hatuna shaka, hata tukikabidhiwa majukumu leo tutayatekeleza kwa weledi na umahiri mkubwa kwa vile yametujengea msingi bora wa utekelelezaji wa majukumu yetu ya kitaalamu na kitaaluma".
#Kupanga ni Kuchagua