Na Mariam Mayunga
Mkuu wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Hozen Mayaya ameishukuru Kampuni ya EcoWater kwa kuweka mashine ya kuuuza maji kwa bei nafuu chuoni hapo, Kampasi Kuu - Dodoma.
Shukurani hizo amezitoa tarehe 14 Mei 2024 wakati wa uzinduzi wa mradi huo hafla iliyoshuhudiwa na wanafunzi wengi wakiongozwa na Serikali yao chini ya Rais wao Bwana Alpha Mshana.
"Mradi huu wa maji safi na salama utakwenda kurahisisha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji safi na salama kwa wanajumuiya wote hususani wanafunzi kutoka kununua lita moja ya maji kwa shilingi elfu moja hadi shilingi mia mbili kwa lita. Hivyo tunawashukuru sana kwa kutuletea mradi huu" alisema Profesa Mayaya na kuongeza " tunajukumu la kuitunza miundombinu ya mradi ili mradi uwe na maisha marefu."
Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo cha Mipango(MISO) Bwana Alpha Mshana akizungumza kabla ya uzinduzi ameishukuru Kampuni ya Eco Water kwa kutekeleza ombi lake kwa wakati. " Nimejawa na furaha siku ya leo kwa kuona ndoto yetu MISO imetimia . Tangu kuingia madarakani, nimetamani kuwa na mradi huu kwa lengo la kuwapunguzia wanafunzi ukali wa bei ya bidhaa hii muhimu kwa maisha ya wanadamu, asanteni sana Eco Water".
Bwana Mshana pia ameushukuru uongozi wa Chuo kwa siyo tu kwa kukubali kuuleta mradi huu chuoni bali pia kwa kurahisisha mchakato.
Katika taarifa yake Meneja wa Mauzo wa Eco Water Bwana Deogratius Masawe amesema Kampuni yao imefanikiwa kusambaza mradi huo katika mikoa 6 nchini ikiwa na jumla ya vituo 17 wanufaika wakiwa taasisi za Umma na binafsi pamoja na wananchi.
#Kupanga ni Kuchagua