Mhitimu wa Stashahada ya Maendeleo ya Jamii katika Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Thabita Pando, akionesha bidhaa anazozalisha.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini wamefanikiwa kujiajiri kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazowaingizia kipato.
Mafanikio hayo yamepatikana baada ya wanafunzi hao kupata mafunzo kupitia Kituo cha Ubunifu na Ujasiriamali cha Chuo cha Mipango maarufu MEI (Mipango Enterpreneurship and Inovation Centre).
Akizungumza na mwandishi wa makala hii Agosti 8, 2023 kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Taaluma Utafiti na Ushauri Elekezi), Profesa Provident Dimoso, amesema MEI ni Kituo Atamizi kwa ajili ya kulea mawazo ya biashara ya wanafunzi na kuwawezesha kufikia ndoto zao.
“Kwa kutambua changamoto ya uhaba wa ajira nchini na duniani kote, Chuo chetu pamoja na kuweka moduli za masuala ya ujasiriamali kwa kila programu, pia tumejiongeza kwa kuanzisha Ktuo cha Ubunifu na Ujasiriamali.
“Vijana wote wanaojiunga na Chuo cha Mipango tunawashauri na kuwahamasisha kujiunga na kituo hicho ili wapate fursa ya kujengewa uwezo kwenye masuala mbalimbali ya ubunifu iwe michezo, sanaa au ujasiriamali ambapo kwa wajasiriamali wanaanzisha biashara mbalimbali, wanajiajiri na kuajiri wenzao,” amesema Profesa Dimoso.
Amesema kupitia program hiyo wanafunzi kadhaa wamefanikiwa kubuni biashara akiwemo aliyeshinda tuzo ya mbunifu bora Tanzania na kudhaminiwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kupatiwa Sh milioni 40 kuendeleza ubunifu wake.
Kijana huyo ambaye kwa sasa amehitimu aliibuka mshindi katika Mashindano ya Maadhimisho ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) mwaka 2021 katika Maonesho yaliyofanyika Viwanja vya Jamhuri, Jijini Dodoma.
MAKISATU huratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kila mwaka yakishirikisha wabunifu kutoka shule za msingi, sekondari, VETA, vyuo vya ufundi, vyuo vya kati, na vyuo vya elimu ya Juu nchini.
Katika hatua nyingine Wizara ya Fedha kwa kuguswa na shughuli za MEI, imeunga mkono juhudi za Chuo za kuwajengea uwezo wanafunzi wajasiriamali kwa kumuongezea mtaji wa Shilingi Milioni Moja mwanafunzi Thabita Pando ili kuendeleza biashara yake.
Akiongea baada ya kupokea msaada huo Thabitha ameishukuru Wizara ya Fedha kwa msaada huo na kuahidi kuongea ubunifu katika biashara yake.
"Nimejawa na furaha kubwa sana. Msaada huu kwangu ni kichocheo cha kunifanya niongeze bidii ya ubunifu na kutafuta masoko ya bidhaa zangu za pilipili na jam," amesema na kuongeza
"Jam ninayotengeneza ina vitamin C ya kutosha, inasaidia kuimarisha mifupa na utunzaji wa ngozi ya mtu,” amesema Thabita ambaye amefaulu vizuri masomo yake ya Stashahada ya Maendeleo ya Jamii na anategemea kujiunga na Shahada ya Kwanza ya Maendeo ya Jamii mwaka huu.
Mwanafunzi huyo amefanikiwa kusajili jina la biashara yake kwa jina la 'Bitha Afrika’ na kutoa wito kwa wahitimu wa kidato cha nne, kidato cha Sita, Astashahada, au Stashahada wenye maono na ndoto za kijasiriamali na ubunifu kujiunga na Chuo hicho wapate fursa za kuendelezwa.
Amesema malengo yake ya baadaye ni kuwa mfanyabiashara mkubwa na kumiliki kampuni.
Kupitia program hiyo wanafunzi huanza kutambuliwa pindi wanapoanza masomo yao na mpaka sasa MEI inalea wanafunzi zaidi ya 40.
Chuo hicho pia huwaombea mitaji ili kuendeleza bunifu zao huku wakiendelea kusoma.